Mpenzi msomaji hizi ni dondoo tu zilizomo ndani ya Somo hili, nimeona ni vema walau kwa sehemu nikueleze yaliyomo ndani.
Mithali 19:14 “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kutoka kwa babaye bali mke mwenye busara mtu hupewa na Bwana’.Nianze kwa kusema kuoa au kuolewa ni mpango kamili wa Mungu. Zipo sababu nyingi za kwa nini unahitaji mke au mume tuanze na:-
1. Unakuwa umejipatia kibali kwa Bwana,
2. Kwa sababu zinaa (1 Wakorintho 7:20),
3. Unapopata mke unakuwa umepata msaidizi na mlinzi. Kibiblia mke /mme mwenye busara mtu hupata kutoka kwa Bwana, maana yake Mungu ndiye anayehusika na kumpa mtu mke/mme. Mungu pekee ndiye anayejua nani ana busara ya kukaa na fulani halafu ndiyo anayekupa huyo mtu. Suala la kumpata mwenzi ambaye hakika ni wa mapenzi ya Mungu kwa mtu husika, imekuwa ni changamoto kubwa hasa kwa vijana na pia wale ambao bado hawajaoa au kuolewa.
Lengo la kitabu hiki ni ;
*kuwasaidia vijana wengi ambao bado hawajaoa au kuolewa kufanya maamuzi sahihi.
*Kuwapa maarifa wale ambao wanafuatwa na vijana wengi kwa lengo la kutaka kuwaoa, nini wafanye pindi wanapofuatwa na vijana wengi.
*Kuwapa uhakika / uthibitisho wale ambao tayari wameshafanya maamuzi haya na tayari wana wachumba kwamba wachumba hao wanatokana na Mungu au la.
*Kuwafariji na kutoa mwongozo kwa wale ambao huenda hamna anayejitokeza kutaka kuwaoa, wanaokataliwa na wale ambao wamechelewa kuolewa halafu wao wanafikiri ni laana.
*Kutoa mwongozo kwa wazazi, wachungaji, walezi, viongozi wa makundi ya kidini kuwasaidia vijana wao katika kufanya maamuzi haya makubwa .
*Kukusaidia kuzipinga hila zote za shetani katika safari hii ya maamuzi.
Kabla ya kuzitaja njia, ndani ya kitabu hicho nimetaja kwanza misingi unayotakiwa kuijua kabla ya kuzijua hizo njia nayo ni;
*Kwa kila jambo kuna majira yake hivyo hata wewe kuoa au kuolewa kwako kuna wakati wako maalumu.
*Mungu hatumii njia au mfumo wa aina moja katika kukujulisha wewe mwenzi wako.
*Mungu anavyo vigezo vya kwake ya kukupa mke au mme ambavyo si lazima viendane na vigezo vya kwako.
*Si kila mke au mme hutoka kwa Mungu.
*Mungu anapoamua kukupa wewe mke au mme anakuwa ameangalia mbali kuliko wewe unavyofikiria.
*Usimuombe Mungu akujulishe mke au mme wako wakati ndani yako umeshajichagulia wa kwako.
*Ni vema uwe umekomaa na umekua kiakili, kiufahamu, na kiroho kwanza kabla ya kufanya maamuzi kama haya na hujaokoka fanya maamuzi ya kuokoka maana ni kwa faida yako mwenyewe.
JE, MAAMUZI YA NANI ATAKUWA MWENZI WAKO WA MAISHA NI YA MUNGU AU YA KWAKO?
Mithali 19:14 “Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; bali mke mwenye busara mtu hupewa na Bwana”.
Ni matumaini yangu kwamba u-mzima kijana mwenzangu na una maendeleo mazuri kiroho na kimwili. Katika waraka huu mfupi kwa vijana nataka kujibu swali hili ambalo vijana wengi wamekuwa wakijiuliza. Wengine kutokana na kutojua ukweli wake wamejikuta wakifanya maamuzi ambayo hadi leo wanayajutia .
Kibiblia, tunajua kabisa ni mpango wa Mungu tuweze kuoa au kuolewa. Sasa swali linakuja, je ni lazima Mungu anionyeshe, anipe mke au mume wa maisha yangu? Kwani mimi kijana sina uwezo wa kuangalia mtu kisha nikaomba Mungu na mwisho nikajichagulia mwenyewe? Au kifupi maamuzi ya nani atakua mume/mke wangu ni ya nani?
Hili ni swali ambalo vijana wengi limekuwa likiwachanganya. Wengine wanaamini maamuzi hayo ni ya Mungu kunipa mke/mume na wengine wanaamini Mungu hahusiki, bali wao ndio wenye nafasi na wanaohusika. Sasa hayo ni mawazo yao wala mimi sitaki kuyapinga lakini ngoja nikuonyeshe Biblia inasema nini halafu utajua ukweli ni upi:-
Kwenye kitabu cha Mithali 19:14 , Mungu anasema suala la nyumba, mashamba, maduka na vyote vifafanavyo na hivi nimewapa uwezo na ruhusa wazazi wako baba & mama) wa mwili wakupe lakini suala la mke au mume mwenye busara mimi pekee ndiye ninaye wajibika kukupa .Sikiliza kama unataka mke/mume kwa ajili ya kulitumikia kusudi la Mungu alilokuumbia basi huna budi ni lazima upige goti kuomba na kisha ungoje Mungu akuonyeshe/ akupe mke/mume wa kusudi lake.
Vijana wengi wanafikiri eti kwa sababu wameokoka, na wamejzwa roho mtakatifu basi wanao – uwezo wa kujichagulia mke/mume wa kuishi nao. Sikiliza kama una amini umeumbwa kwa kusudi la Mungu na unataka kutembea katika njia yake basi mruhusu Mungu akupe mke/mume mwenye busara ya kukaa na wewe.
Mke au mume ana sehemu kubwa katika maisha yako. Anaweza akabadilisha maisha yako, ya kiroho, kiuchumi, kimwili, kihuduma na kima husiano na watu wengine.Hivyo kibiblia maamuzi ya nani atakuwa mkeo au mumeo ni ya Mungu na si ya kwako. Hii ina maana ukimuomba Mungu hakika atakuletea mtu halisi wa kukaa na wewe. Lakini maamuzi ya kumkubali au kumkataa ni ya kwako na si ya Mungu. Ukikubali shauri la Bwana litatumikiwa, ukimkataa, umejikaribishia laana.
Zifuatazo ni sababu za msingi zinazomfanya Mungu akuchagulie/akupe mke/mume na sio kukuruhusu wewe/wazazi/ukoo wako/mchungaji wako kukuchagulia mke.
(a)Kusudi la uumbaji (kuwaunganisha) .
Sikiliza hakuna mtu aliyeumbwa kwa bahati mbaya, Mungu ndiyo aliyekuchagua na siyo wewe uliyemchagua na akakuweka duniani ili umtumikie sasa yeye ndiye anayejua nikimuunganisha huyu kaka na yule dada watalitumikia kusudi langu. Warumi 8:28-29. Mungu anapofanya maamuzi anafanya kwa kuangalia kusudi lake na muda na wahusika wa hilo kusudi. Yeye ni Mungu na anafanya kwa utikufu jifunze kuruhusu mapenzi ya Mungu yatimie na si ya kwako.
(b) Mungu ndiye ana-fahamu nani mwenye busara ya kukaa na wewe.Mithali 19:14b
Busara ni uwezo uliomo ndani ya mtu (mke/mume) unaomsaidia kujizuia kufanya jambo ambalo liko nje ya mpango/mapenzi ya Mungu kwa kufanya lile lilio katika mapenzi yaMungu.Hivyo Mungu pekee ndiye anaye mjua mke/mume mwenye busara ya kukaa na wewe, kamwe wewe hutaweza mjua bila uongozi wa Mungu.
(c) Sababu za ki-Agano.
Zaburi: 32:8 Siku uliyofanya maamuzi ya kuokoka maana yake uliyakabidhi maisha yako kwa Yesu, ukamwambia nafungua moyo wangu uingie uyatawale na kuyaongoza maisha yangu sasa hilo ni Agano lako kwa Mungu. Kwa sababu hiyo Yesu anawajibika kwako kukufundisha na kukuonyesha njia utakayoiendea, hii ikiwa ni pamoja na kukupa mke/mume wa kukufaa.
(d)Mawazo yake, si mawazo yako.
Isaya 55:8 Sikiliza Mungu anayo mawazo (mipango) na njia (mikakati) ya kukufanikisha kimaisha. Sasa katika kutekeleza mipango yake kwako na kupitia wewe lazima atumie mikakati yake ili kutekeleza mawazo yake. Sasa moja ya mikakati yake ni kukupa mke au mume wa kusudi lake .
Sasa, sikatai huenda kwa jinsi ya mwili ni kweli huyo mtu anayekupa Mungu ana upungufu fulani. Huenda umbile lake, sura yake, kabila lake, rangi yake, dhehebu lake, haliko kama ulivyo kuwa unavyotaka wewe. Mungu anakupa mke au mume kutokana na sababu hizo ambazo nimekuekezea hapo juu na ninakuhakikishia ukimkubali atakupa neema ya kukaa naye huyo mtu na kukufanya uridhike naye na kumpenda huyo mwenzako .
Nakutakia uongozi wa Mungu katika eneo la maamuzi ya nani atakua mumeo au mkeo .
RUHUSU MAPENZI YA MUNGU YATIMIE KUHUSU MWENZI WA MAISHA YAKO.
Najua yumkini upo njia panda kwa habari ya kuoa au kuolewa. Si kwa sababu hakuna mtu wa kuoa au kukuoa, bali ni kwa sababu kila anayekuja ni tofauti kabisa na kile ambacho wewe unapenda na unafikiri pia ni mapenzi ya Mungu iwe utakavyo. Huenda kibinadamu kuna sifa/vigezo ambavyo ulijiwekea vya mtu ambaye ungependa kumuoa au kuolewa naye, lakini kila unapoomba unaona mtu anayekuja ni tofauti kabisa na vile ulivyotaka wewe. Na unapoomba zaidi kumhoji Mungu anakuhakikishia kwamba huyohuyo ndiye mtu wa mapenzi yake.
Hukuishia hapo umeshirikisha na wapendwa wenzako au hata watumishi wengine wameomba nao wamethibitisha huyo ndiye mtu wa mapenzi ya Mungu kwako. Kila unapojitahidi kufikiri kumwacha unakosa amani. Mimi ninakushauri inapofika mahali kama hapo we ruhusu tu mapenzi ya Mungu yatimie kwako. Zipo sababu nne za msingi zinazonifanya nikushauri hivyo;
Mapenzi ya Mungu ndio utimilifu wa kusudi lake kukuleta wewe duniani.
Haukuja duniani kwa sababu ni kawaida ya wanadamu kuzaa, bali ni kwa sababu ni Mungu alikusudia wewe uzaliwe.Hii ina maana lipo kusudi la Mungu kukuleta duniani. Na ili kusudi lake liweze kufikiwa ni lazima ujifunze kuishi maisha ya mapenzi yake. Uishi ili kutimiza mapenzi yake hapa duniani.
Ni mapenzi ya Mungu pia kuhakikisha unaoa/kuolewa na mtu ambaye anajua mtasaidiana katika kutekeleza makusudi yake hapa duniani. Kwa hiyo si suala la kuoa au kuolewa unavyotaka, bali ni kuoa au kuolewa kwa mapenzi yake. Mapenzi ya Mungu si lazima yakubaliane/yaendane na ya kwako.
Ni muhimu ujue kwamba mapenzi ya Mungu si lazima yaendane na ya kwako. Na hii ni kwa sababu mawazo yako si mawazo yake na njia zake si njia zako (Isaya 55:8). Jua kabisa mapenzi ya Mungu si lazima yakupendeze, yakufurahishe au yalinde heshima yako. Kuna nyakati ambazo mapenzi ya Mungu kuyapokea ni machungu, yanaliza, yanafadhaisha, yanaogopesha.
Katika kuyakubali au kuruhusu mapenzi ya Mungu yatimie wakati mwingine yanaweza kuwa machungu, kukufadhaisha, kukuliza, kukuumiza, kukuogopesha au hata kukuabisha kwa jinsi ya kibinadamu. Mapenzi ya Mungu yanalenga kuleta heshima na utukufu kwake.
Ingawaje yanaumiza, kufadhaisha au hata kuaibisha kwa jinsi ya kibidamu /kiheshima/kimahusiano/kijamii /kiuchumi nk. Na hata kama kwako yana athari kiasi gani uwe na uhakika mapenzi ya Mungu yanalenga kuleta heshima na utukufu kwake, hii ina maana HAYO NDIYO MAPENZI YAKE na si ya KWAKO. Tunapoomba kusema mapenzi yako (Mungu) yatimizwe ina maana mapenzi/matakwa ya kwetu (wanadamu) yasitimie.
Hebu tuangalie mifano kadhaa ndani ya Biblia;
Mfano wa Yakobo – Mwanzo 29:15-31.
Hii ni habari ya Yakobo alipokwenda Harani kwa Labani nduguye. Labani alikuwa na binti wawili, mkubwa aliitwa Lea na mdogo aliitwa Raheli amabye alikuwa na uso na umbilie zuri. Raheli ndiye ambaye Yakobo alimpenda na alikubali kutumika kwa miaka saba ili apate kumuoa. Baada ya miaka saba, Yakobo alipewa Lea ambaye hakumpenda kama mke bali alimpenda Raheli. Ingawa zilipopita siku saba ndipo alipopewa na Raheli kama mke wa pili.
Nikuulize swali, je Yakobo angeambiwa atumike miaka saba kwa ajili ya kumpata Lea, angekubali? Je unafikiri ni kwa nini Mungu aliruhusu Yakobo mtumishi wake kufanyiwa hili? Sababu kubwa ni hii, ilikuwa ni mpango/mapenzi ya Mungu Yakobo amuoe na Lea pia. Hii ni kwa sababu ya umuhimu wa watoto aliowazaa ukihusianisha na uzao/ukoo wa Bwana wetu Yesu Kristo. Namaanisha kupitia Lea, Yakobo alizaa naye watoto wane, mmoja wao aliitwa Yuda. Ukifuatilia ukoo wa Yesu Kristo utalikuta jina la Yuda linajitokeza (Mathayo 1:2). Kwa hiyo japo Yakobo hakumpenda Lea kabisa lakini Mungu alitaka na akajua kupitia wao atazaliwa Yuda ambaye ni kiungo muhimu katika uzao wa Yesu Kristo.
Mfano wa nabii Hosea – Hosea 1:1-4
Mstari wa pili unasema ‘… Bwana alimwambia Hosea enenda ukatwae mke wa uzinzi…’ Ukisoma hii habari yote utaona jinsi Mungu alivyomwagiza Hosea kwenda kuoa mawanamke mzinzi na aliyekubuhu kwenye dhambi hii. Sasa kwa jinsi ya kibinadamu haikuwa rahisi kulikubali. Lakini kwa sababu ilikuwa ni jambo la MAPENZI YA MUNGU ili mlazimu akubaliane nalo hata kama yeye hakutaka. Na ukiendelea kusoma sura za mbele utaona fundisho na uponyaji ambao ulitokea kwa watu wa taifa la nabii Hosea kutokana na utiifu wake katika mapenzi ya Mungu.
Mfano wa nabii Samweli – 1Samwel 16:1-13.
Hii ni habari inayoelezea agizo la Mungu kwa Samweli kwenda kwenye nyumba ya Yese kumtia mmoja wa watoto wake mafuta kuwa mfalme wa Israel baada ya Mfalme Sauli kuasi. Yese alikuwa na jumla ya wana nane wa kiume, Mkubwa wao aliitwa Eliabu na mdogo aliitwa Daudi. Sasa Samweli alipofika kwa Yese, Yese aliwaita watoto wake wote isipokuwa Daudi aliyekuwa anachunga kondoo wa babaye, akaanza kuwapitisha kwa Samweli ili amtie mafuta yule ambaye ndio mfalme.
Alipopita mtoto wa kwanza, nabii Samweli akasema moyoni mwake Yakini masihi wa Bwana yupo hapa mbele yake, kwa lugha nyepesi alisema yamkini huyu ndiye Mfalme ninayepaswa kumtia mafuta. Je Mungu alimjibu nini alipowaza hivyo moyoni mwake. Mungu alimwambia ‘usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama mwanadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo’. Mwishowe walipita watoto wote saba na Bwana akawakataa, hadi alipofika Daudi aliyetiwa mafuta.
Jifunze yafuatayo kutoka kwenye mifano hii mitatu; Upo duniani sasa kwa ridhaa/ruhusa/mapenzi ya Mungu.
Na kama upo kwa ridhaa yake, ni lazima uishi kwa uongozi wake (Zab 32:8). Thamani ya maisha yako ipo katika kuyatenda mapenzi ya Mungu. Ni kipaumbele (priority) cha Mungu kujua nani atakuwa ni mkeo au mumeo. Sio suala la kuoa au kuolewa unayotaka wewe. Mtazamo wako kuhusu mkeo au mumeo sio mtazamo wa Mungu. Ndoa yoyote anayo iunganisha Mungu ameshaiangalia mpaka mwisho wake.
Hivyo anapokupa mtu wa aina fulani, hata kama haendani na vigezo vyako, kumbuka lengo lake sio kukukomoa au kukuhuzunisha bali ni kuhakikisha anachotaka/mapenzi yake na si ya kwako yanatimia.
Smweli na Yakobo walitaka kukosea kwa sababu ya maumbile na mvuto wa sura kwa nje. Angalia sababu kama hizi zisikufanye ukaharibu mahusiano yako na Mungu na hivyo kukwamisha makusudi yake duniani.
Japo lilikuwa ni jambo gumu kwa Hosea kulikubali kibinadamu, yeye alitii na akabarikiwa kwa kulitumikia shauri la Bwana katika kizazi chake.
Ni mfano wa mfinyanzi na vyombo alivyovifanya. Mfinyazi ndiye anayejua sababu na matumizi ya chombo alichokifanya. Kazi yake huyu mfinyazi ni kuhakikisha lengo la ubunifu/uumbaji wake linafikiwa.
Na Mungu ndivyo alivyo, yeye ndiye aliyekufanya na anajua unachotakiwa kufanya hapa dunani, kazi yake ni kuhakikisha anakuongoza na kukuweka kwenye mazingira ya kusudi lake kupitia wewe kufanikiwa. Sasa mazingira au uongozi huo ni pamoja na kuhakikisha unaoa au kuolewa na mtu wa mapenzi yake.
Mtu wa mapenzi yake anaweza akawa tofauti na ulivyokuwa unataka.
Ndugu yangu inapofika uko mahali kama hapa “the only option/alternative ni kuruhusu mapenzi yake yatimie na si kulazimisha yako kutimia”. This means there is no an option or alternative, you cannot escape it (Je unakumbuka habari za Yona, au Yesu pale Gethesemane?). Let his will be made in your life i.e. Totally submit yourself to his will.
Usipokubali wakati una hakika hayo ni mapenzi ya Mungu kwako maana yake umeasi, ukiasi unatafuta matakwa yako na si yake. Mungu hata kulazimisha kuyatii mapenzi yake ila atakushauri kwa njia mbalimbali na mojawapo na mafundisho kama haya. Ukikataa ushauri wake ujue huko unakoenda yeye/uwepo wake hauko pamoja na wewe. Je unajua gharama ya kukosea au kutokutii mapenzi ya Mungu katika hili? Waulize wanandoa waliokosea ndio utajua madhara yake.
Naamini ujumbe huu umekuongezea maarifa na ufahamu wa kukusaidia katika kufanya maamuzi. Zaidi ni imani yangu kwamba kama ukijua hakika haya ni mapenzi ya Mungu kuhusu mwenzi wako basi utahakikisha yanatimia. Haijalishi hayuko unavyotaka, ndugu zako, ukoo wako, kanisa au hata Mchungaji wako hawamtaki, kama unahakika ni mtu wa mapenzi ya Mungu mpendwa nakushauri RUHUSU MAPENZI YA MUNGU YATIMIE, KINYUME CHA HAPO NI MAJUTO.
“Asomaye na afahamu, msukumo ambao nimeupata kuhusu kuandika ujumbe huu haukuwa mdogo, ni kama nilikuwa naambiwa hakikisha ujumbe huu unakamilika haraka iwezekanavyo ili kuwapa maarifa haya watu wangu”. Mwenye sikio na asikie lile ambalo Roho wa Yesu anasema na kanisa. Amen.
NITAMTAMBUAJE MKE AMBAYE MUNGU AMENIANDALIA?
Swali
Bwana Yesu asifiwe mtumishi wa Mungu.
Awali ya yote napenda kumshukuru Mungu kwa ajili yenu kwa huduma mnayoitoa ambayo imekuwa msaada katika maisha yangu kama mkristo na kama mwanajamii. Mungu awabariki sana. Pili naomba msaada wa maarifa juu ya namna ya kumtambua mke ambaye Mungu ameniandalia. Nimefanya maombi ya kumuomba Mungu mke mwema tangu septemba 2008 hadi sasa lakini bado sijapokea majibu ya maombi yangu.
Ninaamini ninasumbuliwa na tatizo la upokeaji wa majibu ya maombi yangu jambo ambalo linahatarisha ustawi wangu kiroho. Naomba kwa manufaa ya wengine pia ambao wana tatizo kama langu utupatie majibu hayo kwenye kipengele cha maswali na majibu. Ninaomba pia kwa ajili yangu na wengine ambao ninaweza kuwafikia unisaidie majibu hayo kupitia email address yangu hapo juu. Asante sana na Mungu awatimizieni haja za mioyo yenu na kuimarisha huduma yenu ili watu wengi zaidi waimarike kiroho.
Lucas
Majibu;
Hello Lucas, tunakusalimu kwa jina la Bwana, ahsante kutuombea, kututia moyo na kwa swali lako ambalo naamini majibu yake yatawafaa wengi kama ulivyoshauri katika swali lako.
Kaka Lucas swali lako ni pana sana na ‘it is more personal’ kimajibu, lakini namshukuru Roho Mtakatifu anayeweza kutupa majibu ya kutufaa .Katika swali lako nimegundua mambo mawili ya msingi ambayo natakiwa kuyatolea ufafanuzi, moja ni namna unavyoweza kumtambua mke ambaye Mungu amekuandalia na pili namna bora ya kuomba yenye kuleta matokeo. Katika kujibu maswali haya mawili nitazungumzia mambo manne yafuatayo ambayo naamini baada ya kuwa umeyasoma haya utapata ufahamu wa kukusaidia katika kufanya maamuzi hayo yanayokukabili; Jambo la kwanza;
Mungu hatumii njia au mfumo wa aina moja katika kukujulisha wewe mwenzi wa maisha yako (Isaya 55:8). Oktoba 2006 naliandika kitabu kuhusu Njia kumi za Kibiblia zitakazokusaidia kumjua na kumpata mwenzi wako wa maisha. Katika ukursa wa nne wa kitabu hicho ndipo nilipoandika wazo hili hapo juu, kwamba, Mungu hatumii njia au mfumo wa aina moja katika kumjulisha mtu mwenzi wake wa maisha.
Nimeona hata sasa nianze na msingi huu na hii ni kwa sababu vijana wengi hujaribu kuuliza wanandoa waliotangulia kwamba waliwapataje wenzi wao wa maisha kwa dhana ya uongozi wa Mungu? Kutokana na majibu ambayo vijana hao hupewa wengi humuomba Mungu na wanasubiri, Mungu aseme nao kwa njia ile aliyotumia kusema na mtu mwingine.
Kibiblia wazo hili siyo sahihi kwani, Mungu ana njia nyingi sana za kusema na watu wake katika mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na nani atakuwa mwenzi wako wa maisha. Kwa mtu mmoja Mungu anaweza akasema naye kwa ndoto, mwingine kwa sauti yake, na mwingine kwa maono, mwingine kwa mafunuo, mwingine kwa amani ya Kristo, mwingine kwa kutumia watumishi/wachungaji nk.
Jambo ninalojaribu kukuonyesha hapa ndugu Lucas ni kwamba ‘Mungu ana namna yake ya kukusaidia kumtambua mwenzi wako wa maisha, ambayo si lazima ifanane na ya mtu mwingine’. Na mara nyingi namna/njia hiyo haitofautiani sana na ile ambayo Mungu hutumia kusema nawe katika mambo mbalimbali. Hivyo tafuta kujua njia ambayo Mungu huwa anatumia kusema na wewe katika mambo mbalilmbali, naam kwa hiyo aweza kusema na wewe hata kuhusu mwenzi wako.
Jambo la pili; Jenga na kuboresha mahusiano yako na Roho Mtakatifu
Roho Mtakatifu ndiye aliyepewa jukumu la kuwa Msaidizi wako hapa duniani katika kufanya maamuzi mbalimbali. Watu wengi leo wanakwama au wanajikuta wamefanya maamuzi mabaya kwa kosa la kutokumshirikisha Roho Mtakatifu awasaidie.
Mwambie Roho Mtakatifu nahitaji mwenzi(Mke), nisaidie kumtambua yupi ni wa kwangu, naomba uongozi wako. Roho Mtakatifu kwa hakika atakuongoza katika njia sahihi (Zaburi 32:8). Jambo la msingi ni kwa wewe kuboresha mahusiano yako na yake ili kuruhusu mawasilano mazuri kati yenu. Kumbuka mawasilano hutegemea mahusiano. Na jambo la msingi katika kuboresha mahusiano ni utakatifu na kutenga muda wa kuzungumza naye kwa njia ya maombi na neno.
Jambo la tatu; Jifunze kuruhusu mapenzi ya Mungu yatimie kuhusu mwenzi wa maisha yako.
Hili ni jambo lingine la msingi kuzingatia. Endapo umeamua kufuata au kutafuta kumjua mwenzi wako kutoka kwa Bwana, basi ni vema ukaruhusu mapenzi yake juu yako yatimie. Wengi huenda mbele za Bwana wakimuuliza jambo hili lakini anapoleta wazo/jibu lake juu ya nani anafaa, wengi wakishamtazama huyo muhusika kimwili na kwa vigezo vyao humkataa na kusema si Mungu. Ni vizuri ukafahamu kwamba, kama Mungu ndiye aliyemleta mtu wa kwanza kwako na wewe kwa sababu zako binafsi ukasema huyu si wa kutoka kwa Bwana, maana yake umemzuia Mungu asikusaidie kwenye hilo eneo, na hivyo usitegemee kusikia tena kutoka kwake, labda mpaka ujue kosa lako na kuomba toba.
Kumbuka usimuombe Mungu akujulishe mwenzi wako wa maisha wakati moyoni mwako tayari kuna mtu au watu ambao umeshadhamiria kutaka mmoja wao awe mwenzi wako, Mungu hawezi kusema hapo. Ikiwa unataka Mungu ahusike mpe asilimia mia moja hatafanya makosa kama Mwandamu.
Jambo la nne; Jifunze kuomba kimaswali
Najiribu kufikiri kwa nini umeomba tangu Septemba 2008 hadi sasa Mungu asijibu? Kwa ufahamu nilionao katika Kristo nina hakika yeye alisha-kujibu ila wewe ndiyo hukuelewa kwamba alijibu. Nina uhakika huo kwa sababu mtu amwendeaye Mungu kutaka kujua jambo, Mungu humjibu mtu huyo ili kumsaidia asipotee katika jambo hilo.
Naamini shida ipo kwako, huenda jibu ulilokuwa unataka wewe ni kuambiwa fulani ndiye mwenzi wako, kumbe kwa Mungu huenda alikuwa anasema huu si muda wake endelea kuomba maana kwa kila jambo kuna majira yake. Zaidi huenda shida iko kwenye namna unavyoomba na namna unavyopokea, au kuelewa Mungu anapoleta jibu.
Ili kuweza kupata ufumbuzi juu ya jambo hili jifunze kutumia mfumo wa maswali katika maombi yako, naamini utaona matokeo yake. Jifunze kuyatengeneza maombi yako kimaswali, omba huku ukitaka kujua/ukitafuta ufumbuzi wa lile unaloliombea kwa Mungu.
Jambo la msingi katika maombi haya ni kuwa na muda wa utulivu wa kuhojiana na kusemezana na Mungu wako. Kama vile ambavyo unaweza kuongea kwa simu na rafiki yako na mkasikilizana na kujibizana, ndivyo Mungu anavyotaka tujifunze kuwasilama naye. Unaeleza haja yako kwa swali na unampa muda na yeye akujibu. Najua kama hukuwa na mazoea ya kutumia mfumo huu, unapoanza itakusumbua, lakini endelea kufanya hivyo utona matokeo yake.
Ingawa swali lilikuwa ni pana, naamini Roho Mtakatifu ameniongoza kujibu kwa namna ambayo kwako Lucas na hata msomaji mwingine mwenye changamoto kama hii, mtakuwa mmepata ufahamu wa kusaidia. Kama umefuatilia kwa makini katika majibu yangu sijeleza moja kwa moja ni kwa namna gani utamjua mwenza wako, ila nimeelezea mazingira mbalimbali ambayo ukiyazingatia itakuwa ni rahisi kwako kumjua mwenzi wako wa maisha. Kupata ufahamu juu ya njia za Kibilia za kumjua na kumpata mwenzi, wasiliana nami nitakutumia kitabu bado nina nakala chache naamini kitakusaidia pia.
Na:Patrick Sanga Mungu akubariki, tuzidi kuombeana.
Kwa Nini Uchumba ni “Mtamu” Zaidi Kuliko Ndoa Kwa Walio Wengi?
1. Wapendwa wanaJF, kwa wale waliowahi kupitia hatua ya uchumba hadi kufikia ndoa au hata wale ambao hawajawahi kupitia hatua hizo, lakini wameona mifano kadhaa kwenye jamii, watakubaliana na mimi kwamba ndoa nyingi “zinaumwa” na zinahitaji kutafutiwa “chanjo” au “tiba!”
2. Naamini kwamba kabla ya kufikia ndoa wachumba huwa wanavumiliana na kupendana mno, kila mmoja anamwona mwenzake ni bora kuliko yeye! In fact kama hawajaonana siku inakuwa haijaenda sawa!
3. Lakini baada ya kuingia kwenye ndoa mambo hubadilika taratibu na kuanza kuleta kero, malumbano yasiyoisha, huzuni zisizoisha, ngumi, mateke, n.k. Kuna baadhi ya wachungaji huwa wanatumia usemi huu ufuatao wakati wanafungisha ndoa: “Wengi wa walio ndani (ya ndoa) wanaka watoke na walio nje (ya ndoa) wanataka kuingia!” Kwa maana hiyo ndoa ni taasisi ya ajabu sana!
4. Swali langu ni kwamba kwa nini uvumilivu, upendo, huruma, kujaliana, (ambao mimi nimeuita “utamu”) nk ambako kunaonekana kwenye uchumba usiendelee hata wakati wa ndoa?
5. Lengo la mada hii ni kujaribu kuwasaidia wenzetu ambao wanataka kuingia kwenye ndoa pamoja na wale walioko kwenye ndoa ili waweze ku-“think twice” na kutengeneza mahusiano yao ili maisha yao yawe na ushuhuda mbele ya jamii na watoto (kama wamefanikiwa kuwapata).
6. Kwa kuanza kutoa maoni, kwa upande wangu naona kwamba (a) wengi wanaingia kwenye mahusiano kwa sababu ya “tamaa za mwili” kiasi kwamba wanaangalia uzuri wa nje zaidi kuliko wa ndani! Uzuri wa nje ukishaanza kuchuja upendo nao unaanza kuchuja vile vile! (b) Kingine ni kwamba baadhi ya watu (hapa nafikiri ni wengi zaidi) huwa wanaingia kwenye mahusiano kwa sababu ya kuangalia vipato zaidi kuliko upendo wa dhati, uchumi ukianza kuyumba, ndoa nako inaanza kuyumba na hatimaye kuvunjika!
USHAURI: Upendo wa kweli usiathiriwe na mazingira: uzuri, kipato na kadhalika! Hii ni sumu mbaya katika ndoa! Naomba maoni yenu zaidi.
JIFUNZE KUFIKIRI KABLA HUJACHUKUA UAMUZI WA KUOA AU KUOLEWA
Nawasalimu kwa jina la Yesu . Leo katika nyanja hii ya vijana, nimeona ni vema tukashirikishana kuhusu suala la ‘kufikiri kabla ya kuoa au kuolewa’.
Siku moja katika kusoma Biblia nilikutana na mstari ufuatao, nakusahuri uusome kwa umakini. Biblia katika 1Wakorinto 7:8-9 inasema “Lakini nawaambia wale, wasiooa bado na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo, lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe, maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa”.
Baada ya kuusoma mstari huu niliingia katika tafakuri nzito sana ambayo mwishowe ilinipeleka kuandaa somo hili, kwamba ni vema ukafikiri vizuri kabla ya kuchuka uamuzi wa kuoa au kuolewa.
Unajua malezi, dini, madhehebu yetu, wazazi, mila na desturi vinachangia kwa kiwango kikubwa sana kuhusu utaratibu wa kuanzia mtu kupata mke au mume mpaka watakapofunga ndoa. Kila kundi lina mfumo na utaratibu wake ambao lingependa vijana waufuate ili kuhakikisha wanaoa na kuolewa kwa kile ambacho kila kundi linaona na kuamini kwamba huo ndio uataratibu mzuri kufuatwa.
Namshukuru Mungu kwa kuwa nami nimeoa, ingawa vitu vingi sana Bwana alikuwa ananifundisha vinavyohusu ndoa hata kabla sijaoa. Nakubaliana na dhana kwamba ili uweze kuwa Mwalimu mzuri kwenye nyanja fulani basi ni lazima au ni vema wewe mwenyewe ukawa umepitia kwanza kwenye nyanja hiyo. Lengo ikiwa sio tu ufundishe ‘theory’ bali pia utufundishe na uzoefu wako binafsi kwenye eneo hilo. Licha ya kukubaliana na dhana hii, kwangu binafsi haikuwa hivyo, maana kuna mambo mengi ambayo, Bwana Yesu, alikuwa ananifundisha yanayohusu ndoa hata kabla sijaoa.
Kwa kifupi ndoa ni shule au darasa ambalo wanandoa wanatakiwa kukaa chini na kujifunza kila siku namna ya kuishi humo ndani ili kuweza kuishi maisha ambayo Mungu amewakusudia.
Kutokana na mifumo ya baadhi ya makanisa yetu, si vijana wengi ambao wanafundishwa kwa undani kuhusu maamuzi haya makubwa. Wengi wao wameingia kimwili na kujikuta wakijutia na kulaumu kwa nini nilimuoa au kuolewa na huyu kijana. Nasema haya kwa kuwa nimekutana na wanandoa wengi wa aina hii, na nataka nikuambie kama Biblia ingetoa mwanya wa wanandoa kuachana na kuoa au kuolewa na mtu mwingine, wapendwa wengi sana walioko kwenye ndoa wangefanya hivyo na wengine wasingekubali kuolewa au kuoa tena.
Unajua kwa nini?
Ni kwa sababu si vijana wengi wenye ufahamu wa kutosha juu ya aina ya maamuzi wanayotaka kuyachukua. Kwa hiyo katika somo hili nimeona vema niandike mambo manne ya msingi ambayo naamini yataongeza na kupanua ufahamu wako ili kukusaidia kufikiri kwanza kabla ya kufanya maamuzi haya makubwa;
Si kila ndoa inayofungwa imeunganishwa na Mungu, kwa kuwa ndoa ni kiungo cha muhimu kwa Mungu na Shetani pia.
Kuanzia mwaka 2005, Mungu alinipa kibali cha kuanza kufundisha na pia kushauri juu ya mambo kadhaa kuhusu wanandoa. Tangu wakati huo hadi sasa nimekutana na baadhi ya wanandoa ambao wanajuta kwa nini walikubali kuoa au kuolewa. Wanaishi kwenye ndoa kwa sababu tu ya watoto na pia kwa hofu kwamba endapo kama wataachana jamii na watu wanaowazunguka hawatawaelewa.
Ni vizuri ukafahamu kwamba si kila ndoa inayofungwa ni ya mapenzi ya Mungu, hata kama imefungwa kanisani. Biblia inaposema kilichounganishwa na Mungu, mwanadamu asikitenganishe, katika nafasi ya kwanza maana yake iwe ndoa ambayo Mungu ndiyo aliyehusika katika kuanzisha mahusiano na kuwaongoza hao watu kuishi pamoja. Wakati Mungu anatafuta kuhakikisha watu wake wanaoana katika mapenzi yake na Shetani naye anapambana kuhakikisha watu wanaoana katika hila (mapenzi) zake.
Shetani amefanikiwa kwa kiwango kikubwa sana kuvuruga wanandoa wengi na kuwafanya waishi maisha tofauti na yale ambayo Mungu aliwakusudia. Ni kwa sababu hii ndio maana Paulo aliwaambia Wakorinto ‘Lakini nawaambia wale, wasiooa bado na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo, lakini ikiwa hawawezi kujizuia, na waoe, maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa’. Paulo aliona shida, maudhi ya wandugu walioko kwenye ndoa tokana na migogoro aliyokuwa akikutana nayo.
Fahamu kwamba ni furaha kubwa kwenye ufalme wa giza mtu anapooa au kuolewa kinyume cha mapenzi ya Mungu. Hii ni kwa sababu Shetani anajua akifanikiwa kukushawishi ukaoa kinyume na mapenzi ya Mungu, ameharibu ‘future’ yako na kile ambacho Mungu alikusudia ukifanye hapa duniani. Kumbuka suala sio kuoa au kuolewa tu, bali ni kuingia kwenye ndoa ambayo itakuwezesha kulitumika shauri la Bwana katika kizazi chako. Hivyo kabla hujaamua nani uishi naye hakikisha unamshirikisha Mungu akuongoze kumpata mwenzi sahihi.
Unapaswa kuoa au kulewa katika mapenzi ya Mungu
Naam kuoa au kuolewa katika mapenzi ya Mungu ni changamoto nyingine kubwa kwa vijana wa kizazi cha leo. Naam hili ni eneo ambalo Mungu yupo makini sana kufuatilia nani atakuwa mwenzi wako wa maisha. Na upande wa pili nao, Shetani anapigana kwa juhudi kubwa ili kuvuruga kusudi la Mungu kupitia mtu au watu.
Ni vizuri ukafahamu kwamba unapotaka kufanya maamuzi ya kutaka kuoa au kuolewa, Shetani naye ataleta mawazo (mapenzi) yake ndani yako juu ya nani anafaa zaidi kuwa mwenzi wako maisha. Lengo lake ni kuhakikisha anakuunganisha na mtu ambaye anajua kwa huyo atakumaliza kiroho na kihuduma kabisa. Suala sio kuwazuia msiende kanisani, bali ni kuhakikisha kile ambacho ungefanya kwa kuwa na mtu sahihi hakifanikiwi. Ukitaka kujua ukweli wa jambo hili, muulize Mchungaji wako, kesi nyingi anazokutana nazo kanisani kwake zinahusu nini, naamini atakujibu kimapana. Ni jukumu lako kuwa makini kufuatilia unatii wazo la nani, Mungu au Shetani?
Vigezo vya kimwili ni silaha kubwa ya uharibifu
Vigezo vya kimwili ni moja ya silaha kubwa ambazo Shetani anazitumia kuwavuruga watu wengi waweze kuoa au kuolewa nje ya mapenzi ya Mungu kwao. Jifunze kufukiri na kutafsiri mambo au makusudi kama Mungu anavyotazama na kutafsiri. Na uwezo wa kufanya hili utaupata kwenye neno lake tu. Kwako mwanaume Mungu anapokupa mke anakupa Mlinzi na msaidizi. Na kwa mwanamke Mungu anakuwa amekupa kichwa. Ni muhimu sana kuchunga ni msaidizi, mlinzi au kichwa gani unataka kiunganishwe na maisha yako kwa njia ya ndoa.
Ndoa ni wajibu mkubwa
Ndani ya ndoa kuna wajibu mkubwa sana unaokusubiri kama baba au mama. Ndani ya ndoa muda na uhuru wako unabanwa na mwenzi wako. Ndoa inabana pia muda wa kuwa na Mungu wako. Na kwa wengi kwa kutaka kuwapendeza zaidi waume au wake zao, wamefarakana na Mungu, kwa sababu wamewapa waume au wake zao hata nafasi na muda wa Mungu kwenye maisha yao.
Usiingie ndani ya ndoa kwa fikra za uapnde mmoja. Naam ndoa ni wito wa mapungufu na uvumilivu ambao ni lazima uwe tayari kuchukuliana na mwenzi wako katika mapungufu yake. Kuna vitu hamtaweza kufanana na kwa sababu ya mapungufu yaliyopo kwa kila mmoja unapaswa kutafakari kuhusu majukumu yanayokuja kwako kama mwanandoa, hekima na busara katika kuzikabili changamoto za ndoa, kama vile kuzaa au kutokuzaa, kutokujiweza katika masuala ya unyumba, matumizi ya fedha, tabia za mwenzi wako nk.
Haya ni mambo ya kuhakikisha unayaombea mapema ili kujenga msingi imara utakapoingia kwenye ndoa yako. Lakini nikutie moyo kwamba endapo utaoa au kuolewa katika mapenzi ya Mungu, yeye ni mwaminifu, atakuunganisha na mtu ambaye katika changamoto mtakazokutana nazo hazitawakwamisha wala kuwafanya mjute. Bali endapo Shetani ndiye ataongoza maamuzi yako, ni majuto makubwa sana (asomaye na afahamu).
Mungu akubariki, naamini ujumbe huu umeongezea mambo ya kutafakari na kuzingatia kabla ya kufanya uamuzi wa kuoa au kuolewa.
HASARA ZA KUFANYA TENDO LA NDOA KABLA YA NDOA.
Andiko la Msingi ni Mithali 5:1-20.
Mungu ndiye aliyewaumba mtu mume na mtu mke, akawaweka bustanini ili wamtumikie. Mungu akamuumba mwanadamu na kumpa viungo mbalimbali katika mwili. Akawapa wanadamu maungo maalumu kwa ajili ya tendo la ndoa na kisha akaliweka tendo la ndoa kuwa takatifu, tena la halali kwa wanandoa tu, tena hasa wale waliounganishwa na yeye.
Sasa katika kizazi cha leo tunaona watu wengi hasa vijana ambao bado hawajaoana (kwa maana ya kuwa wanandoa) vijana hao wanafanya tendo hilo la ndoa (ngono) tena kwa uchafu usio wa kawaida, wanafanya kwa kuzidi mipaka ambayo Mungu amempa mwanadamu, maana yake wanatumia isivyo (mis-use) maumbile/ maungo ambayo Mungu amewapa.
Soma warumi 1:24-27.Sasa wao wanapofanya haya hawajui kwamba kuna hasara kubwa wanayoipata na wao wanafikiri ndio wanakwenda na dunia. Lengo la ujumbe huu ni kukueleza hasara za kufanya tendo la ndoa kabla ya ndoa nazo ni;
(1)Ni dhambi.
Kufanya ngono kabla ya ndoa ni dhambi na warumi 6:23a inasema mshahara wa dhambi ni mauti; na pia katika Ezekiel anasema Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa, hivyo kwa sababu hiyo hicho kitendo kitakusababishia kifo cha kimwili na kisha utahukumiwa tu na mwisho kutupwa jehnamu
(2)Kuwashibisha wengine nguvu zako.
Mithali 5:10 Tendo la ndoa ni tendo linalohitaji mtu atumie nguvu, hivyo kadri mtu (hasa mwanume) anapofanya mara kwa mara anajipotezea nguvu zake anawashibisha wengine nguvu zake na hivyo dhoruba itamkuta katika ndoa yake pindi atakapooa kwa sababu hatakua na nguvu tena kama awali.
(3)Utavunjiwa heshima.
Mithali 5:7, Siku zote yule unayefanya naye tendo la ndoa kwanza atakuona wewe ni mpumpavu kwa sababu anajua afanyaye tendo hilo hana akili kabisa (mithali 6:32) kwa hivyo atakudharau, zaidi atakutangaza kwa wengine na wewe mwenyewe pindi utapooa au kuolewa kwa kuwa nguvu zako uliwashibisha wengine basi utavunjiwa heshima na huyo mwenzi wako.
(4)Unafanya jambo litakaloiangamiza nafsi yako.
Mithali 6:32. Nafsi kwa kiyunani inaitwa Psuche, ndani yake kuna hisia, akili na maamuzi ya mtu. Hivyo kuiangamiza nafsi yako ni kuangamiza future yako na mipango yako uliyokuwa umejiwekea ya mbele.
(5)Unajitengenezea majeraha na fedheha maishani.
Mithali 6:33. Sikiliza katika ngono unaweza ukapata kilema cha maisha, na magonjwa ya hatari kama vile kaswende, ukimwi n.k. Haya magonjwa yatapelekea nyama na mwili wako kuangamia utashindwa kufikia malengo uliyojipagia, utabakia kujuta tu na watu watakufanyia fedheha na wakati huo upo kitandani hujiwezi.
(6)Kuwapa wengine miaka yako.
Mithali 5:9 , Uchunguzi chunguzi unaonyesha kwa mtu anayependelea kufanya ngono mara kwa mara hasa anapoanza kabla ya ndoa mara nyingi hawezi kuishi kwa muda mrefu si hivyo tu lakini pia tumeona mara nyingi vijana wakijiua/wakiuana /wakifa kwa ajili ya mapenzi, wengine wanaugua hadi wanakufa wadogo na kupatwa na magonjwa mabaya, na hivyo muda waliostahili waishi hapa duniani na hivyo wanakuwa wamewapa wengine miaka yao.
(7)Kuvamiwa na maroho machafu.
Katika kufanya ngono, wengine wanaenda hadi kwa waganga wa kienyeji na wachawi na huko wengine wanapewa madawa ya ajabu ambayo yanapelekea kuwamiwa na mapepo ya ajabu, na wengine kwa kupenda ngono wamefanya ngono na majini bila wao kujua na tayari yamesha wamiliki na hawaji watatokaje kwenye kifungo hicho.
Mimi nimekuonyesha hasara zile za kibiblia tu, sasa zipo za kijamii, kitaifa, kifamilia nk. Naamini baada ya kuwa umesoma ujumbe huu, kama bado unafanya ngono basi utabadili tabia yako na kuacha ngono mpaka wakati utakapo fika na kama haujaokoka nakusihi uokoke ili Yesu akupe nguvu za kushinda hiyo dhambi. Kama unataka kuokoka bonyeza category ya wokovu kisha utapata maelekezo ya kufanya.
Bwana Mungu akulinde na kukutunza.
EmoticonEmoticon